ZIJUE FAIDA ZA MAHINDI YA NJANO KWA MAMA MJAMZITO

Kwa mujibu wa taarifa za majarida mbalimbali ya lishe, ambazo zinathibitishwa pia na mtaalamu wa lishe nchini, Linus Gedi, ni kwamba mahindi hayo yamejawa na virutubisho vyenye faida nyingi zikiwamo za wingi wa vitamin A zinazosaidia kuzuia upofu na kuimarisha utimamu wa mama mjamzito na kichanga chake baada ya kujifungua.
Faida nyingine za mahindi hayo ni pamoja na utajiri wake wa wanga, vitamin, protini, madini na viinilishe vingine muhimu katika kuukinga mwili dhidi ya magonjwa kama ya kisukari, maradhi ya moyo, pia kuzuia saratani mbalimbali zikiwamo za matiti na ini.
Faida ambazo si za kusahauliwa pia ni pamoja na kulinda chupa ya uzazi ya mama mjamzito, kusaidia mchakato wa kumeng’enya chakula mwilini na ukuaji wa watoto.
Uchunguzi umebaini kuwa mahindi hayo, siyo tu yanasaidia kupatikana kwa mlo wa uhakika, bali pia hufanya kazi sawa na dawa au kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali. Inaelezwa kuwa kwa kawaida, kina mama wajawazito hulazimika kupewa dawa za kuwaongezea vitamin A kwa faida yao na watoto wao tumboni, lakini ulaji mzuri wa mahindi lishe ya rangi ya chungwa (njano), hupunguza au kuondoa kabisa ulazima wa kutumia dawa hizo.
Utafiti wa hivi karibuni uliowahi kufanywa na Dkt. Wendy White wa Chuo Kikuu cha Iowa, Idara ya Sayansi ya Chakula na Lishe ya Binadamu nchini Marekani, uligundua kuwa mahindi ya njano (rangi ya chungwa) ni chanzo kipya cha uhakika wa kupata vitamini A.
Katika utafiti huo, wanawake sita wenye afya walipatiwa aina tofauti ya ugali wa mahindi, ambapo mmoja ulikuwa wa mahindi ya rangi ya chungwa na mwishowe ilibainika kuwa mahindi ya rangi ya chungwa yaligeuzwa kuwa vitamini A karibu mara mbili ya kiwango kilichokuwa kikifahamika kuwamo katika mahindi ya kawaida hapo kabla. Aidha, tafiti nyingine za mwaka 2010 zilionyesha kuwa upungufu wa vitamini A umeenea miongoni mwa watu wa mataifa yanayoendelea na kusababisha watoto takribani 500,000 kupata upofu kwa mwaka duniani na pia kuongezeka kwa hatari ya magonjwa na vifo; mambo ambayo hudhibitiwa pindi mahindi ya njano yanapotumiwa kwa usahihi.
MTAALAMU
Linus Gedi alisema kuwa mahindi ya rangi ya chungwa, yana kiwango kizuri cha vitamin A na hivyo kuwa na msaada mkubwa kwa walaji, hasa kina mama wajawazito ambao pia huhitaji ziada ya Folic Acid inayopatikana kwenye virutubisho vya mahindi hayo ili kuondoa uwezekano wa kuzaliwa watoto wenye uzito mdogo.
“Mjamzito anatakiwa kula vyakula vinavyomwongezea vitamini A badala ya kula vidonge. Anaweza kuongeza vitamini A mwilini kwa kunywa uji wa mahindi ya rangi ya chungwa ambayo yana virutubishi vingi na bora zaidi kwa afya yake na mtoto,” alisema.
Alitaja faida nyingine za ulaji wa mahindi hayo kuwa ni pamoja na kuimarisha mifupa na pia kupunguza kuwa na mwelekeo wa kunenepa kupita kiasi. Aidha, inaelezwa kuwa mahindi ya njano (chungwa) siyo tu huupa mwili nishati na vitamin A, lakini pia huupatia mwili vitamin B, vitamin E na madini mengi yakiwamo ya magnesium, zinki, chuma, shaba na selenium.
ULAJI
Inaelezwa kuwa ulaji wa mahindi ya njano au chungwa upo wa aina nyingi, lakini ule wa kupata virutubishi zaidi ni pamoja na kuhusisha mahindi mabichi na tena yaondolewe maganda wakati masharubu yake yakiwa bado hayajakauka. Aina mojawapo ya mapishi ni pamoja na kuyachemsha na mlaji akiamua anaweza kuongeza ndimu, pilipili na chumvi kwa nia ya kuongeza ladha. Pia supu yake inafaa kwa afya, au chembe zake kutumiwa kama sehemu ya saladi.
HT @ Nipashe
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post