ZIJUE TABIA 13 ZINAZOWAPA MAFANIKIO WABUNIFU WENGI DUNIANI

Ubunifu ni dhana ngumu kidogo kuielezea ukaeleweka. Kufikiria kibunifu ni jambo ambalo wengine wanalimudu bila shida yoyote lakini pia yawezekana ikawa hali tofauti baada ya mabadiliko ya mazingira. Mawazo ya kutengeneza kazi ya ubunifu yawezekana yakaonekana kuibuka kutoka pasipojulikana lakini baadaye yakapotea kabisa katika wakati ambao ungeyahitaji zaidi. Kufikiria na kuweza kuibuka na wazo la kibunifu kunahitaji utofauti wa fikra lakini si kama kufikiria tunakofanya wengi wetu.
Tafiti zinaonesha kwamba ubunifu unajumuisha mkusanyiko wa tabia, mawazo na msukumo wa kijamii vyote viwemo ndani ya mtu mmoja.
Ingawa hakuna aina maalum ya watu “wabunifu,” kuna baadhi ya tabia za watu wanaoonesha ubunifu wa hali ya juu kabisa katika kazi zao au maisha yao. Hizi ni baadhi tu ya tabia hizo:
Wana ‘ndoto za mchana’
Walimu wengi wamejikuta wakiingia kwenye historia mbaya za wanafunzi wenye ubunifu wa hali ya juu kwa kuwaambia kwamba hayo wanayoyawaza ni ‘ndoto za mchana’ (kuwaza mambo ambayo kwa wengi yanaonekana hayawezekani kufanywa) ni kujipotezea muda. Wabunifu wengi wanajua kwamba hili linalosemwa na walimu wao si la kweli japokuwa kwa wakati huo wanaweza wasijue jinsi gani ya kuweza kuwathibitishia hivyo walimu wao.
Wengi wetu tunajua kutokana na matukio yaliyowahi kututokea kwamba mawazo ya maana na ya kibunifu zaidi yanaibuka tu kutoka kusikojulikana wakati mawazo yetu tukiyaelekeza sehemu nyingine.
Mawazo haya yanayoitwa ‘ndoto za mchana’ na wengine yanaweza kumsababisha mtu aunganishe matukio kwa sababu akili ina uwezo wa kukumbuka taarifa zote hata kama mtu yupo kwenye vikwazo. Wataalamu wa mfumo wa fahamu wamebaini kuwa ‘ndoto za mchana’ zinashughulisha/kusisimua sehemu ile ile ya ubongo inayohusika na ubunifu.
Wanachunguza/kudadisi kila kitu
Dunia ni maabara kubwa kwa wabunifu — wanaona uwezekano wa kila wanaloliwaza na jinsi linavyoweza kutekelezeka na muda wote wanakuwa wanaingiza mawazo mapya na taarifa ambazo wanaweza kuzionesha kwenye kazi zao za kibunifu. Kwa wabunifu wengi, hakuna jambo jipya ambalo kwake linakuwa halina maana au likakosa matumizi.
Hii ndio sababu baadhi ya watu huwa na vitu vitavyowawezesha kuhifadhi mawazo yanayowajia muda wote. Vitu kama kalamu na karatasi au simu ambavyo hutumia kuhifadhi mawazo mapya na yanayoweza kutumika kwenye kazi zake za kibunifu.
Wanajipangia muda wa kufanya kazi
Wasanii wengi wakubwa au wenye majina makubwa wameshawahi kukaririwa wakisema kwamba kazi zao nyingi zilizotamba nyakati za asubuhi sana au usiku sana. Wengi wamekaririwa wakisema kwamba hufanya kazi zao nyingi mpaka usiku sana na kulala karibu na alfajiri au asubuhi kabisa. Bila kujali muda gani wanafanya kazi, watu wenye mafanikio kwenye kazi zao za ubunifu mara nyingi hujichunguza na kubaini muda ambao wanakuwa na uwezo mkubwa wa kufanya ubunifu huo – tofauti na mpangilio maalum wa ajira za wengi ambapo muda wa kufanya kazi unawekwa na waajiri wetu.
Huunganisha matukio
Kama kungekuwa na jambo moja tu linalowatofautisha watu wenye ubunifu kwa kiwango cha juu na watu wengine, basi ingekuwa ni uwezo wao wa kuona fursa za kutimiza mawazo yao – uwezo ambao wengi wanaukosa — kwa lugha nyepesi, waweza kuuita mtazamo wa mbali. Wasanii wengi wakubwa pamoja na waandishi wamesema kwamba ubunifu ni uwezo wa kuunganisha matukio na mawazo ambayo wengine hawatawahi kuwaza kuyaunganisha au kuyatafutia uhusiano wake.
Kutumia maneno ya Steve Jobs, muanzilishi wa kampuni ya Apple:
“Ubunifu si jambo jingine bali ni kuweza kuunganisha mawazo na vitu. Unapowauliza wabunifu wengi ni vipi walifanya jambo fulani, wengi wanapata hisia za “kuwa na hatia” kwakuwa kikweli hawakufanya lolote, wanakuwa waliona jambo tu na kulitekeleza. Kwao jambo hilo linaonekana kuwezekana hasa baada ya kuliangalia na kulitafakari kwa muda. Hii ni kwa sababu wanaweza kuunganisha mawazo waliyowahi kuyapata sehemu mablimbali.”
Hutenga muda wa kuwa peke yao
Ili uweze kuwa wazi kufanyia kazi mawazo ya kibunifu lazima uwe na uwezo wa kuwa peke yako na kuutumia muda huo kupata mawazo yenye manufaa. Ni lazima mtu aweze kushinda woga wa kuwa mpweke.
Wasanii na wabunifu wengi mara nyingi sana wamekuwa wakiitwa ni watu wapweke, na ingawa yawezekana kuwaelezea hivi isiwe sahihi, wanapokuwa peke yao ndio muda wanaoutumia kwa kiasi kikubwa kuweza kufanikisha ubunifu wao mwingi – huku kwa wengine wanaoangalia wanaweza kusema kuwa ni upweke. Wengi wao wanakubali kwamba unahitaji kutenga muda wa kuwa peke yako ili uweze kuruhusu akili yako kuwaza vitu mbalimbali vitavyokuwezesha kubuni jambo fulani.
Unahitaji kujiongelesha wewe mwenyewe na kuja na majibu ambayo unaweza kuyafanyia kazi. Ni ngumu sana kuweza kufanikisha hili endapo hutengi muda wa kujiongelesha wewe mwenyewe, na hii ndio tofauti kubwa kati ya wabunifu na wengine.
Wanageuza vikwazo wanavyokumbana navyo kuwa fursa
Watu wengi wenye mafanikio makubwa wamewahi kusema kuwa mafanikio yao yametokana na kuweza kuendelea wakiwa wamekumbana na maumivu na kukatishwa tamaa na wengi wanaowazunguka — na kwamba wametumia changamoto hizi kama sababu ya kutaka kufanikisha shughuli zao ili kuwaonesha waliowapinga kwamba hawakuwa sahihi au hawakuwa wakiona alichokuwa akikiona yeye. Hivi karibuni watafiti walibaini kwamba matatizo makubwa yanaweza kuwasaidia watu waweze kuwa bora zaidi kwenye mahusiano na watu wengine, imani kwa Mungu, kuthamini maisha zaidi, kuwa watu tofauti kabisa, na muhimu zaidi — kuwa wabunifu — kuweza kuona fursa mpya za kimaisha unapobanwa na matatizo.
Watu wengi wanaweza kutumia changamoto walizokumbana nazo kuwawezesha kuja na njia mbadala ya kuzitatua. Mambo yaliyowahi kuwatokea maishani na kuwafanya waache kuiona dunia kama walivyokuwa wanaiona awali – kuwa ni sehemu salama sana au kila unachokitaka kinaweza kujileta kumesababisha waiangalie dunia kwa upeo mwingine kabisa wa kibunifu.
Wanatafuta uzoefu mpya
Wabunifu wengi wanapenda kujiweka kwenye mazingira mapya mara kwa mara, kuanza kufurahia starehe mpya au kuanzisha uhusiano mpya — na tabia hii ya kujiweka wazi kwa mabadiliko ni muhimu sana kwa kazi za ubunifu.
Hii yaweza kuhusisha vitu mbalimbali lakini vinavyohusiana kwa karibu: Mawazo mapya ya kiakili, starehe au kuwa wazi kwa hisia zako za kimwili. Jambo linalowauganisha wabunifu wengi ni uhitaji wa kuziwezesha akili na tabia zao kuweza kuuvinjari ulimwengu, ulimwengu wako mwenyewe na unaokuzunguka.
Huinuka haraka wanapojikwaa na kuanguka
Usugu waliojitengenezea wa kuweza kuendelea na shughuli zao wanapokuwa wameanguka ni tabia muhimu sana inayowahakikishia kufanikiwa wabunifu wengi. Kufanya kazi za kibunifu mara nyingi husemwa kuwa ni mchakato wa kushindwa mara kwa mara mpaka utakapopata mbinu yenye mafanikio, na wabunifu — walau kwa wale wenye mafanikio kwenye kazi zao za kibunifu — wameshaweza kufanya makosa kuwa ni sehemu tu ya mafanikio yao ya baadaye.
Wanapenda kuzungukwa na mazingira/ vitu vizuri
Wabunifu wengi wanathamini sana vitu vizuri na kwa sababu hiyo wanapenda wazungukwe na mazingira ya aina hiyo.
Utafiti uliofanyika hivi karibuni na kuchapishwa kwenye jarida la “Psychology of Aesthetics, Creativity, and the Arts” umeonesha kuwa wanamuziki — wakiwemo wale wanaopiga vyombo peke yake, walimu wa muziki — wameonesha uwezo mkubwa sana wa kibunifu wanapowekwa kwenye mazingira wanayoyapenda ambayo yametawaliwa na vitu vizuri sana.
Wanafanya shughuli wanazopenda
Wabunifu wengi huwa wanahamasika wao wenyewe kufanya kazi zao bila kusukumwa na mtu mwingine — ikimaanisha kwamba hamasa au msukumo huu wanaoupata unatokea ndani mwao, na si hamasa ya kuwawezesha kutambulika au kupewa zawadi. Wanasaikolojia wameonesha kwamba wabunifu wengi wanapata hamasa kubwa wakiwa na jambo gumu la kutafutia jawabu, ikiwa ni ishara ya kupata msukumo kutoka ndani na tafiti zimethibitisha kwamba kwa kuwa na msukumo wa ndani tu wa kufanya jambo, yatosha kabisa kuhamasisha ubunifu.
Wanaangalia na kudadisi watu
Wakiwa ni wadadisi wakubwa kiasili na wenye shauku kubwa juu ya maisha ya watu wengine – hasa mafanikio na matatizo yao, wabunifu wanapenda kuangalia watu wengine — na wanaweza kujikuta wakipata mawazo bora kabisa ya kazi zao kutokana na kufanya hivyo.
Hawajali wanafanya kazi kwa muda mrefu kiasi gani
Wabunifu wengi wanapokuwa wanafanya kazi zao – iwe ni kuandika, kucheza, kuchora, kupaka rangi au kujielezea kwa njia yoyote ile, wanakuwa katika hali inayowawezesha kuwa wabunifu katika kiwango cha juu kabisa. Hii ni hali ambayo wanasayansi wanasema kuwa inawawezesha wabunifu kuhamisha fikra zao kufikia uwezo wa juu wa kubuni bila kutumia nguvu za ziada za akili. Mtu anapokuwa kwenye hali hii anakuwa hawezi kujua mambo yoyote yanayoendea nje au ndani ambayo kwa kawaida yangemsukuma kuwaza kufanya kitu tofauti na kuathiri ubunifu wake.
Unaweza kuwa katika hali hii endapo utakuwa unafanya jambo unalolipenda sana na ambalo una uwezo mkubwa sana wa kulifanya kwa ufasaha, lakini ambalo pia linakupa changamoto kubwa — kama ambavyo kazi yoyote kubwa inayohitaji ubunifu inavyokuwa.
Kutoka nje ya mawazo ya kawaida
Wanasaikolojia wanasema kwamba lengo jingine la ‘ndoto za mchana’ ni kutusaidia kutoka nje ya mawazo yetu ambayo yana upeo mdogo sana na kuweza kuuvinjari na kuja na njia mpya za kufikiria, ambalo linaweza kuwa ni jambo bora sana katika kazi za ubunifu.
‘Ndoto za mchana’ zinatuwezesha kujitoa kwenye wakati na mahali tulipo sasa. Sehemu hiyo hiyo ya ubongo inayohusika na ‘ndoto za mchana’ ndio inayohusika na kutuwezesha kuwaza maisha ya baadaye na pia kutuwezesha kufikiria mtu mwingine atakuwa anawaza nini.
Tafiti zimethibitisha pia kuwa kuweza kujiwekea “umbali wa kisaikolojia” — ikimaanisha kuweza kutumia mawazo au mtazamo wa mtu mwingine kuhusu jambo unalolifanya kana kwamba analitatua yeye — litaongeza sana ubunifu na kufikiria.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post