CHADEMA WAKAIDI AMRI YA POLISI KUHUSU TUNDU LISSU

Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) limetangaza kuwa kesho Jumapili Septemba 17 litaendelea na maombi kwa ajili ya Tundu Lissu licha ya Polisi kupiga marufuku mikusanyiko yote iliyopanga kufanya maombi.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo jioni, BAVICHA wamesema kuwa, wameendelea na maandalizi ya shughuli ya Maombi ya Kitaifa ya Vijana Kumuombea Tundu Lissu ambaye hali yake bado si nzuri, akiwa chumba cha uangalizi maalum, Hospitali ya Nairobi, nchini Kenya.
Kama ambavyo baraza liliutanganzia umma kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA (Bara), Patrick Ole Sosopi, maombi hayo (National Youth Prayer for Lissu), yanatarajiwa kufanyika Jumapili, Septemba 17, mwaka huu, katika Uwanja wa Tip, Sinza darajani, jijini Dar es Salaam.
Kupitia Kamati ya Maandalizi, BAVICHA inapenda kuwaambia Watanzania wote ambao watapenda kuhudhuria maombi hayo kuwa maandalizi yote muhimu yameshafanyika kwa ajili ya kuhakikisha shughuli hiyo ya kiimani inafanyika kama ilivyopangwa.
Aidha, kutokana na taarifa za baadhi ya vyombo vya habari leo, BAVICHA ingependa kusema yafuatayo kuhusu shughuli hiyo ya kumuombea uponaji Lissu;
1. Hadi sasa tumezingatia taratibu zote za kisheria ambazo zinatuelekeza kutoa taarifa kwa mamlaka za kiserikali, hususan Jeshi la Polisi. Kwa sababu hadi sasa jeshi hilo halijatuandikia barua ya kutuita ili kujadiliana nao kuhusu kufanikisha shughuli hiyo, tunaamini kuwa hawana pingamizi lolote la kiutaratibu kama ambavyo sheria inaelekeza.
2. Tumefuatilia kwa kina kuhusu kauli za Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ambazo zimenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari leo ikidhaniwa kuwa amezuia shughuli hiyo ya maombi, na tumebaini kuwa ZPC Mambosasa hakueleweka vyema, kwa sababu aliulizwa swali kuhusu shughuli yetu ya kumuombea Lissu, lakini yeye akatoa majibu kwa kuzungumzia maombi ya maandamano ya watu walioomba kibali cha kuwapokea wabunge wao wakiwa wanatokea Dodoma, ndiyo maana akazungumzia maandamano. Tumejiridhisha tena kuwa taarifa tuliyopeleka kwa jeshi la polisi kama sheria inavyoelekeza, tukiwataarifu kuhusu maombi hayo, haikutaja wala kuzungumzia maandamano bali watu wa dini mbalimbali zilizopo nchini wanaoguswa na tukio la Lissu na maumivu anayopitia hospitalini, watakutana na kuomba sala/dua ili Mwenyezi Mungu afanye uponyaji kwa mgonjwa wetu.
3. Tunapenda kusisitiza kwa mara nyingine tena, BAVICHA tumefanya kazi ya kuratibu tu maombi hayo, lakini itakuwa ni shughuli ya kiimani, ndiyo maana tumealika viongozi wetu wa kiroho waje kusimamia na kuendesha maombi hayo ya kumuombea ndugu yetu Lissu.
Kwa wito huu, tunawasihi na kuwaomba watanzania wote wa Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kuja kumuombea ndugu, rafiki, mwanachama na kiongozi wetu Mhe. Tundu Lissu, pamoja na taifa kwa ujumla.
Tunaendelea kuwahamasisha vijana na wananchi mbalimbali wanaoguswa na mwito wa kushiriki maombi hayo ya kumwombea Lissu kufika uwanjani hapo kuanzia saa 8 mchana.
Madaktari wanatibu, Mungu anaponya.
Imetolewa Leo,
Tarehe 16.09.2017
___________________
Julius Mwita
Katibu Mkuu
BAVICHA.
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post