MCHEZO WA AZAM, SIMBA SASA KUPIGWA SAA 10.00 JIONI

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limefanya mabadiliko kidogo ya muda wa kuanza mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kati ya Azam FC na Simba SC.

Mchezo huo utafanyika leo Jumamosi Septemba 9, 2017 kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salam kama ulivyopangwa awali.

Kuhusu muda, mchezo huo ulipangwa ufanyike kuanzia saa 1.00 usiku, lakini sasa utaanza saa 10.00 jioni - uamuzi uliofanyika baada ya kupokea ushauri kutoka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda.

Mbali ya mchezo huo, mechi nyingine ya kesho Jumamosi Septemba 9, mwaka huu itakuwa ni kati ya Tanzania Prisons na Majimaji ya Songea uliopangwa kufanyika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mechi nyingine za Ligi Kuu ya Vodacom, zitakuwa Jumapili Septemba 10, mwaka huu ambako Njombe Mji FC na Young Africans SC zitacheza Uwanja wa Sabasaba mjini Makambako wakati Mtibwa Sugar FC na Mwadui FC ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro.

Kadhalika Lipuli FC itacheza na Stand United FC Uwanja wa Samora mjini Iringa wakati Singida United itacheza na Mbao kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Pia Kagera Sugar itacheza na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba huku Mbaya City ikiwa wenyeji wa Ndanda ya Mtwara kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

TAARIFA KUHUSU WA WAAMUZI TANZANIA

Kamati ya Utendaji ya Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) ilikuwa na kikao chake cha kwanza kilichofanyika Julai 6, 2017 hapa jijini Dar es Salaam.

Mambo muhimu yafuatayo yalitolewa uamuzi.

1. Kumpongeza Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Bw. Wallace Karia na Makamu wa Rais, Bw. Michael Wambura pamoja na Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuchaguliwa kwao.

2. Tumesimamisha kozi zote kwa waamuzi wapya kuanzia Septemba 7, mwaka huu. Mitihani iliyokwishafanywa kabla ya Septemba 7, mwaka huu ni halali na itumwe kwa Katibu Mkuu wa FRAT - Taifa mara moja ikiambatanishwa na ada zake.

3. Makatibu wote wa FRAT - Mkoa kwa mikoa yote ya Tanzania Bara wakumbushwe majukumu yao kwani inaonekana ni kama wamepitiwa ikiwa ni pamoja na kutuma kwa Katibu Mkuu FRAT - Taifa orodha ya waamuzi wote wa madaraja yote walio hai kwa kuchezesha na walio hai kiuanachama.

4. Tumekumbusha waamuzi kuwa na darasa la mara moja kwa wiki lijulikanalo kama ‘Sunday Class’ madarasa hayo yawe kila Makao Makuu ya Mkoa na Makao Makuu ya Wilaya.

5. Tumekubaliana uchaguzi mdogo ufanyike wakati wa mapumziko ya ligi ya wiki mbili za mwezi Januari. Tayari tumewasiliana na na Kamati ya Uchaguzi.

6. Kuwaleta pamoja waamuzi (wanachama) wote nchini bila kujali umri.

7. Kuendelea kuzalisha waamuzi wapya toka kwenye shule za sekondari, vyuo na nje ya shule za sekondari na vyuo kwa wenye sifa.

8. Kuboresha mafunzo na upandaji wa madaraja kwa waamuzi wenye madaraja.

9. Kukemea na Kupambana na rushwa kwa waamuzi hadharani kwa kushirikiana na TFF na Takukuru.

10. Kutetea kwa nguvu zote haki za waamuzi.

11. Kuboresha mawasiliano kwa ngazi zote na kwa mwanachama ye yote.

12. FRAT kiwe chama cha mfano kwa wanachama wake kwa kuwa na maadili mema, yanayompendeza Mungu.

13. Misingi kumi ya “FIFA FAIR PLAY” ni msingi wa maendeleo ya mwamuzi.

14. Wote kwa pamoja tukatae rushwa na tuiangamize rushwa kwa maendeleo ya mpira wetu.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
JIUNGE NA ZOTEKALI BLOG
Katika FACEBOOK, TWITTER, INSTAGRAM ili kupata habari zetu kirahisi install app ya ZOTEKALI BLOG HAPA
HTML tutorial

Sambaza habari kwa marafiki

Author:

Best Tanzania, Africa and World News Blog, Gossip, Entertainment, Life and Health Tips, Employment and Opportunies,Celebs life and Scandals..... Updated Daily .

Previous Post
Next Post